Spread the love

Upepo mwanana wavuma kwa utulivu, miti aina ya mikalatusi na Mipera inatabasamu kwa kucheza kwa madaha isharatosha kuwa ilikuwa siku njema.

Nje ya Kasri yetu ya msonge na duara iliyokandikwa kwa udongo na kuezekwa nyasi, nimeketi mkekani nikibugia busara kutoka kwenye kitabu cha mwandishi tajika duniani. Nilizama katika utamu wa hadithi iliyosukwa kwa ubunifu na utaalam wa upeo wa juu zaidi hadi nikasahau kupiga mafunda ya uji kutoka katika bakuli langu wakati huo wa kishuka. Jua lilizidi kuvutwa na magharibi nami sikubisha kusonga palipo na kivuli. Mhusika mkuu wa hadithi ni Msanifu Kombo ila wengi wanamfahamu kama Kongowea Mswahili. Mamake Kongowea anaitwa Zainabu Makame. Yeye ni mtiribu na alijulikana sana na wengi katika tasnia ya mziki hasa mashairi ya taarab. Kongowea hajui babake aliko licha ya kudokezewa kwa ufifi tu na mamake alipokuwa anakata kamba. Bi Saumu rafiki yake mkaza mjomba baada ya kuokolewa na Kongowea kutoka katika mikono ya fahali anaamua kumfichulia siri Kongowea kuhusu babake nayo inakuwa mwanzo wa siku njema.

Babake Kongowea aliitwa Juma Mukosi, kisanii akaitwa Ajum Isokum naye alikuwa mkazi wa Kitale kijiji cha Makutano kwa Ngozi. Mkaza mjomba na ubinafsi wake awali walipanga njama ya Kumleta Enock Minja aende achukue nafasi ya Kongowea ila anafia Mombasa katika ajali. Kongowea anaanza safari ya kujisaka ili ajue mshtakabali wa maisha yake. Licha ya visa na dhoruba hapa na pale, ikiwemo kusakwa na Suleiman Mapunda ambaye ni adui ya Kongowea tangu skulini hadi Mombasa, na kifo cha Rashid ambaye alikuwa rafiki yake wa dhati pale Mombasa, Kongowea anaendelea na safari yake. Anaabiri gari hadi Nairobi na kuchukua lingine hadi Kitale. Hajui aendako ila anajua majina ya sehemu anakoenda. Baadaye, anatua katika hoteli moja mjini Kitale. Anakutana na mama mmoja na bintiye na baadaye kuandamana nao hadi Makutano kwa Ngozi. Anakuwa wa msaada sana katika kumfunza binti yule lugha hadi kiwango cha kualikwa skulini Suwerwa kuzungumzia ushairi. Njiani anakutana na mzee kazikwisha. Baadaye mzee anamwalika kwake. Kongowea alisahau mwaliko wa mzee na kukumbuka baada ya wiki mbili.

Wakati huo, mawingu meusi yanakaribisha mvua wa baraka. Kongowea anafika kwa Mzee Kazikwisha. Anakaribishwa na harufu ya mzoga na nzi waliokuwa katika sherehe. Mzee aliaga ila alimwachia barua kuwa yeye ndiye aliyekuwa babake yake Kongowea na historia nzima ya ujana wake pamoja na uhusiano na mamake, Zainabu Makame. Kongowea alikuwa na hisia msemo. Si furaha, si simanzi. Alipokea hati miliki ya mali ya babake. Ikawa ameiona siku njema, akajua mshtakabali wake na kuishi kwa raha na kumbukumbu.

Nagutushwa ghafla kuwa kitabu kimefika mwisho. Hakuna kurasa zingune. Narudi kwenye Blabu. Imeandikwa, ‘Siku Njema’ Ken Walibora. Baridi ya jioni iliniamsha mkekani nikahisi nimesafiri kwote kama Kongowea. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa mimi kutaka kujua kuandika kama Ken. Ni uchu sio tena mshawasha. Nilirudi kumaliza kula uji wangu kwa furaha.

Na Prince Frank

Leave a Reply

avatar
  Subscribe  
Notify of